Sura ya 1 - Matunda

Je, umewahi kujiuliza maswali haya: Mungu anatarajia kwamba nitapata ushindi kwa njia gani hapa duniani? Ninapaswa kuishi namna gani? Kwa nini sipati ushindi mkubwa zaidi? Iwapo Mungu yupo kwa ajili yangu, kwa nini basi maisha yangu hayaonyeshi hivyo? Nimesikia juu ya nguvu za Mungu, lakini labda alinisahau mimi alipokuwa akiwapa wengine nguvu zake. Katika Yakobo 2:5 imeandikwa hivi: “Ndugu zangu wapenzi, sikilizeni, Je, Mungu hakuwachagua maskini wa dunia wawe matajiri wa imani na warithi wa ufalme aliowaahidia wampendao?” (maana ya neno maskini ni: mtu asiye na mali, uwezo, kazi, heshima, anayeishi bila msaada, asiye na nguvu ya kutimiza lengo lake, ombaomba, anayeomba sadaka).

Sisi sote tunayo mahitaji halisi. Makubwa kati ya hayo ni haya: upendo, usalama na umuhimu. Ndani ya mahitaji hayo, tunayo mahitaji mengine yaliyo wazi zaidi. Baadhi ya watu wanahitaji chakula na mavazi, wengine wanahitaji watoto wao wamjue Mungu, wengine wanahitaji kuponywa magonjwa, na mahitaji mengine kadha wa kadha.

Vyakula na mahitaji yetu yapo katika uwepo wa Mungu

Biblia inasema katika Wafilipi 4:19 kwamba, “Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.” Iwapo Mungu anakwenda kukujaza kila unachokihitaji katika “utukufu”, inabidi utafute mahali utukufu wake ulipo, na kisha umngojee Mungu kwenye utukufu huo. Vinginevyo huenda unamngojea Mungu mahali pasipostahili. Nikingojea basi katika stesheni ya treni, siwezi kulipata. Inabidi nitafute mahali kituo cha basi kilipo! Sisi nasi tunatakiwa kutafuta mahali utukufu ulipo. Neno “utukufu” linapohusishwa na Mungu linamaanisha uwepo wake. Tunahitaji kwenda katika utukufu wake, kumsikiliza anaponena nasi Neno lake. Neno lake hugeuka kuwa ahadi na mbegu iliyopandwa katika mioyo yetu na hatimaye itazaa matunda kama

"Mungu akawabarikia, akawaambia, Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha; mkatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi. Mungu akasema, Tazama nimewapa kila mche utoao mbegu, ulio juu ya uso wa nchi yote pia, na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu."

(Mwanzo 1:28-29).

Yesu alikuwa akituambia tubadilike, tutubu hali ya kujitahidi sana kujitosheleza kimahitaji, tuwe wazaaji wa matunda.

"Tokea wakati huo Yesu alianza kuhubiri, na kusema, Tubuni; kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia." (Mathayo 4:17). Huko ndiko kubadili mwelekeo. Utakapofanya hivyo, utaona ufalme wa Mungu uko karibu nawe sana kiasi kwamba unaweza kuushika.

Huenda unauliza, alikuwa anamaanisha nini? Tuache nini? Ufalme wa Mungu ni nini? Ninaamini kwamba tunapaswa kuacha njia za kidunia za kuishi maisha na badala yake tufuate njia ya ufalme wa Mungu. Naamini kwamba jambo hili linahusu maisha yetu yote. Naamini pia kwamba Yesu hakuwa akiwaambia tu watu hawa, "acheni kufanya dhambi na pia tubuni njia zenu mbaya." Hapana, Yesu alikuwa akitupatia mpango wa jinsi ya kuishi.

Wanadamu hutumia kanuni zote za kidunia na za kujitosheleza wao wenyewe ili kutimiza mahitaji yao. Mahitaji yetu ya msingi ni upendo, usalama na umuhimu(kuwa watu wa maana).

Je, Petro hakuandika kwamba ahadi za Mungu zinatukirimia vitu vyote kwa ajili ya uzima na utauwa? Soma 2 Petro 1:3-4.

Watu wanaposhindwa kutimiza mahitaji yao hawataki kuukubali ukweli huu kwamba dunia kamwe haitawapa mahitaji yao. Wanajaribu kuziba pengo kwa kujitahidi kujiendeleza wenyewe, wakitumaini kuwa mambo yatakuwa mazuri. Hufikiri kwamba lazima kuna kosa fulani katikati yao. Hatimaye hujiona wana hatia na kuanza kuzifikiria vibaya tabia za Mungu. Shetani naye huzidi kuwadanganya na wao hukubaliana na uongo wake. Na kisha huona mashaka juu ya ukweli wa Neno la Mungu.

Kwa hiyo jibu ni nini? Tunawezaje kuupata ufalme wa Mungu kwa kugeuka au kuacha njia fulani? Yesu alisema katika Marko 4:11 kwamba siri ya ufalme wa Mungu imefunuliwa katika mfano wa kupanda na kuvuna. Kupanda na kuvuna nini? Kupanda na kuvuna Neno la Mungu!

Matokeo ya mwisho ya kulima ni kupata matunda

Yesu alisema katika Marko 4 kwamba ufalme wote wa Mungu hufanya kazi katika kanuni hii. Alisema kwamba hii ni siri ya ufalme. Siri ni ipi? Kwamba maisha huendelezwa na Neno la Mungu lililopandwa katika moyo wa mtu. Halafu kinachofuata ni hatua za kukua. Pamoja na ukuaji huo kuna maumivu. Maumivu yanayotokana na Shetani anayejaribu kuliiba Neno wakati unapomngojea "Bwana arudi" na matunda.

Anasema kwamba tunahitaji kuwa watu wanaotegemea Neno, wasiojitegemea, wala kuutegemea ulimwengu. Njia ya kumtegemea Mungu ni kutegemea nguvu ipitayo kawaida ya Neno la Mungu!

Hatuhitaji kuwa wajuzi sana katika kuyashughulikia maisha kama jinsi tunavyohitaji kuwa wajuzi katika kushughulika na Neno la Mungu.

Kwa maneno mengine tunasema: tubu (yaani, acha yale unayoyaamini na kuyategemea kwa ajili ya mahitaji yako mazito, acha kujitegemea mwenyewe na kuutegemea mfumo wa dunia) kwa sababu Ufalme wa Mungu (yaani utaratibu wa Mungu ulioelezwa katika Marko 4 wa kupanda mbegu ya Neno la Mungu katika moyo wako, na kuiacha ikue ili izae kila kitu unachokihitaji kwa ajili ya maisha na utauwa, na kwa kuzaa matunda kwa utukufu wa Mungu) sasa uko karibu nawe.

Iruhusu neema ya Mungu itawale maisha yako

Utafute kwanza Ufalme wa Mungu, na haki yake; na yote unayoyahitaji utazidishiwa, yatakufunika kama jinsi matunda yanavyofunika tawi la mzabibu (Mathayo 6:33).

Katika Matendo 26:18 tunasoma kwamba tunapogeuka au kutubu, tunajiondoa kutoka katika nguvu za Shetani na kujiweka chini ya nguvu ya Mungu.

Aina tatu za matunda Mojawapo ni kwa kila tunachohitaji na kila anachohitaji Mungu

1. Tunda la Roho: Tunda la ndani. Hili ni tunda linalokufanya ufanane na Yesu. Soma Wagalatia 5:22-23. "Lakini tunda la Roho ni

14

upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria."

2. Tunda kwa ajili ya maisha yetu: Hili ni pamoja na tunda la kijamii, kifamilia, kiafya na kimwili, kifedha, nk. Katika 1 Wakorintho

9:7 imeandikwa hivi: "Ni askari gani aendaye vitani wakati wowote kwa gharama zake mwenyewe? Ni nani apandaye mizabibu asiyekula katika matunda yake? Au ni nani achungaye kundi, asiyekunywa katika maziwa ya kundi?"

3. Tunda la Kimisionari: Tunda kwa ajili ya wengine; yaani huduma. Neno la Mungu katika Yohana 4:36 linasema: "Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja."

Matunda yote yana mbegu ndani yake kwa ajili ya kuzaa. Katika Mwanzo 1:11 imeandikwa: "Mungu akasema, Nchi na itoe majani, mche utoao mbegu, na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, juu ya nchi; ikawa hivyo."

Mara tunda la ndani linapokuwa ndani yetu, humwaga nje mbegu zinazozaa tunda la nje, au huduma kwa wengine.

Kanuni ya mbegu au Neno inatendaje kazi?

Katika Marko sura ya 4:1-21 tunaelezwa juu ya mfano wa mpanzi. Ufalme wote wa Mungu hutenda kazi katika siri hii. "Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu, bali kwa wale walio nje yote hufanywa kwa mifano." (Marko 4:11).

Katika mfano huu Yesu alitupatia utaratibu rahisi wa kufuata ili tuenende katika ufalme wake katika hali ya kuzaa na kumpendeza

Hakuna ubaguzi wa rangi, elimu, umri, jinsia, akili, hadhi ya kijamii au kifamilia. Hakuna!

Soma Marko 4:1-21. Katika Marko 4:11 tunapata maneno yafuatayo "Akawaambia, Ninyi mmejaliwa kuijua siri ya ufalme wa Mungu." Katika Marko 4:14 imeandikwa pia hivi: "Mpanzi huyo hulipanda neno."

Hutenda kazi sio tu kama mbegu, bali pia kama punje ya haradali

Katika Marko 4:30-32 tunasoma pia maneno yafuatayo: "Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? au tuutie katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake."

Punje ya haradali ni punje inayojulikana kuwa ndogo sana kuliko zote. Mbegu nyingine zote za mboga za majani huota na kuwa mimea lakini punje ya haradali huota na kuwa mti! Sio jambo la kawaida kitu kinachoonekana kidogo kuzaa kitu kikubwa! Vile vile sio kawaida mmea wa msimu kuwa mti. Ndivyo ilivyo kwa mbegu ya Neno la Mungu na Ufalme wa Mungu. Haionekani kubwa, lakini itakupatia mahitaji yako yote, kama jinsi punje ya haradali inavyofanya kwa ndege wa angani. Soma Luka 17:5 kuhusu imani ya punje ya haradali.

Kila mtu lazima achague mojawapo ya njia hizi za kuishi

Ufalme wa Dunia Ufalme wa Mungu

Shetani ni mfalme Tunakuwa watumwa wake Tunatumia akili zetu kukidhi haja zetu Tunaishi kwa kufanya vitu visivyo na thamani katika maisha ya milele

Yesu ni mfalme Tunakuwa watumwa wake Tunatumia Neno lake kukidhi haja zetu matunda Tunaishi kwa kufanya vitu vitakavyotupatia thawabu katika maisha ya milele.

Lakini angalia! Ili tunda likue, kuna kanuni au utaratibu. Kanuni hii isipofuatwa, tunda litakufa. Tunayo mambo mawili tu ya kuchagua: Kukua au Kufa!

Hii ndiyo dhamira ya "Kukua au Kufa." Ni kanuni ya Mungu ya kuzaa matunda.

1) Tunahitaji kuligeukia Neno kwa ajili ya matunda 2) Tunahitaji kujua jinsi ya kutoka nje na kukaa mbali na hali ya kuwa Wafungwa katika nchi ya Ahadi. 3) Tunahitaji kujua jinsi ya kumkaribia Mungu -Hali hii ni Mto

Utiririkao. 4) Tunahitaji kujua zaidi kuhusu tabia ya Mungu - Mungu ni nani. 5) Tunahitaji kujua sisi ni kina nani hasa katika Yesu – KUKETI

6) Tunahitaji kuuchukua msalaba wetu na kutembea kwa kulitii Neno – KUENENDA

7) Tunahitaji kujua juu ya adui yetu Shetani na jinsi anavyokuja kuliiba Neno; na jinsi ya KUMPINGA hadi ushindi na matunda yanapopatikana.

Haya yatakuwa masomo katika mfululizo wa Kukua au Kufa. Ni masomo ya Kibiblia, yanatenda kazi, yanahusu kile ambacho Neno linafundisha, na ninaweza kushuhudia kwamba kamwe Mungu hajashindwa kutumia kanuni au hatua hizi katika maisha yangu.

Katika Yohana 15:18-27 Yesu anatuonya kwamba sehemu ya hatua za kuzaa matunda ni kuchukiwa na kuteswa, lakini pia Roho Mtakatifu yupo kama mfariji wetu.

“Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu.” (Yohana 15:20). Watu wengi hawapati wanayoyahitaji kwa sababu Shetani au wasaidizi wake huja na kuliiba Neno kabla halijazaa matunda. Tunahitaji kujua kwamba kuchukiwa, majaribu na mateso tunayoyapitia hayamaanishi kwamba tunda halikui, kinyume chake, mambo hayo ni dalili kwamba tunda

linakua. Tunahitaji kuwa wenye hekima!

Mbegu zinahitaji chakula. Zinahitaji maji na madini. Tunahitaji kuongezea hayo kwenye mbegu iliyopandwa.

Kuna kanuni ambayo kwayo mtu anayemwamini Yesu Kristo hukua.

Kuielewa kanuni hiyo na njia na kushirikiana na Mungu katika hiyo, kutahakikisha kwamba mtu anayemwamini Yesu atakua. Tunaamini kwamba kozi hii ya Kukua au Kufa ina maji, vitamini na madini

yanayohitajika kwa ukuaji.

Kuwa mjinga, na au kukataa kushirikiana na Mungu, kutamfanya mtu anayemwamini Yesu awe “Mfungwa katika nchi ya Ahadi”.

Wana wa Israeli walifanikiwa kuingia Nchi ya Ahadi. Katika kitabu cha Waamuzi, watu wa Mungu, ingawa walikuwa katika agano na Mungu, walikuwa wafungwa kwa maadui zao. Gideoni na watu wake ni mifano kwetu ya wafungwa waliopata kuwa huru.

Kwa namna hiyo hiyo, watu wa Mungu siku hizi ni wafungwa wa hofu, hatia, ulevi, kuhukumiwa, kiburi, majivuno na maadui wengi wa kiroho.

Njia ya kuepuka kukaa kifungoni, ni Kukua!

Mwisho wa hatua za kukua ni Matunda. Matunda ni matokeo ya kukaa ndani ya mzabibu utakaotoa ”mmisionari” ndani ya kila mtu amwaminiye Yesu Kristo. Angalia katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana, matokeo ya mwisho baada ya vita vyote ni Matunda.

Kuna makundi 7 makubwa katika hatua za Kukua au Kufa

Kuzaa Matunda Wafungwa katika Nchi ya Ahadi Mto UtiririkaoMungu ni naniKuketiKuenendaKupinga (Lengo la kuzaa matunda)

(Hali tunayoweza kuwa nayo) (Ushirika na Mungu) (Tabia yake) (Nafasi yetu katika Kristo) (Wajibu wetu)

(Ushindi wetu katika vita)

Hayo ndiyo “Masomo 7 ya Mwongozo” yanayofanya Sehemu ya 1 Semina ya 1. Sehemu ya 2 Semina ya 2 ina masomo mengine 4 yanayohusu Msalaba, Pepo na Ukombozi na Ubatizo wa Roho Mtakatifu.

Kila kundi hapo juu lina masomo kadhaa ambayo mwanafunzi anaweza kujifunza ili akamilishe kozi ndefu. Katika kozi ndefu, utaanza kwa masomo yaliyoorodheshwa hapo juu, kisha utaendelea na masomo mengi yaliyomo ndani ya baadhi ya makundi hayo makuu. Kwa mfano, kundi la Mungu ni nani lina masomo 18. Kuketi lina masomo 13, Kuenenda lina masomo 41, na Kupinga lina masomo 11 (kuna masomo zaidi katika Kozi ya 3). Unaweza kuchagua kutoendelea na kozi baada ya kusoma na kujifunza masomo 11 katika kitabu hiki au unaweza kuendelea kukamilisha kozi yenye masomo zaidi ya 90.

Ni muhimu kwetu kujua jinsi tunavyojifunza na jinsi tunavyotenda mambo ya kiroho. Hatujifunzi mambo ya kiroho kama tunavyojifunza mambo ya kidunia, kwa njia ya habari au taarifa tulizo nazo katika akili zetu. Ni kweli kwamba akili zetu pia ni sehemu ya njia inayotumika kujifunzia mambo hayo.

Hata hivyo huwa tunapokea ufunuo kwa Mungu, yaani tunapokea kitu kilichofunuliwa ambacho awali kilikuwa kimefunikwa au hakikuwa kinaonekana. Shetani huweka utaji kwenye macho yetu ya kiroho ili tusiweze kuona (Wakorintho 4:4). Lakini jambo kubwa kabisa linalotupasa kujua ni kwamba, tunapopokea ufunuo huu, tunaupokea kama mbegu, na siyo kama tunda. Hivyo kwa kila sehemu ndogo ya ukweli ambao Bwana hutufunulia, tunapaswa kuuweka katika utaratibu au kanuni ya Mungu ni nani, Kuketi, Kuenenda na Kupinga. Mungu hutufunulia jambo fulani kuhusu yeye mwenyewe, kisha huliweka jambo hilo katika maisha yetu (Kuketi), kisha tunahitaji kutii na kuenenda katika jambo hilo. Kwa uhakika Shetani huja kuiba Neno, hivyo tunapaswa Kumpinga. Tukifanikiwa kufanya hivyo tutazaa matunda. Ukisoma Marko sura ya 4 utaona maandiko yanayoelezea jambo hilo.

Kwa hiyo utaratibu huu wa uanafunzi wa Yesu, sio tukio moja kubwa katika maisha yetu. La hasha, ni utaratibu unaoendelea tunaoupitia siku hadi siku, kwa kila kipindi cha maisha yetu. Utaratibu huu kamwe hauna mwisho. Tunaweza kupinga suala moja lakini wakati huo huo tukawa katika kanuni au utaratibu wa kuketi katika suala jingine la maisha yetu.

Ufuatao ni muhtasari wa mtaala wa Kukua au Kufa

Tunda (Somo hili). Kuutumainia Ufalm wa Mungu; Neno la Mungu.

Mto Utiririkao. Tunahitaji kufanya tawi liendelee kuungana na mzabibu kwa njia ya ushirika. Tunahitaji uwepo wa Mungu katika maisha yetu ya kila siku. Hii ni ramani rahisi ya kibiblia kwa ajili ya kufanya hivyo katika muda wako binafsi wa kumwabudu Mungu. Sura ya 47 ya kitabu cha Ezekieli inaeleza juu ya mto unaotiririka kutoka katika hekalu la Mungu na kwenda katika bahari iliyopotea ya wanadamu. Sisi ni hekalu la Mungu. Kuwa karibu na Mungu hutangulia huduma ya kweli!

Wafungwa katika Nchi ya Ahadi. Tunahitaji kuwa huru ili tusiwe matawi yatakayotupwa katika moto wa kutozaa matunda. Gideoni ni mfano wa Mwisraeli aliyekuwa na agano na Mungu, akiishi katika nchi ya ahadi, aliyopewa na Mungu, lakini bado alikuwa mfungwa kwa maadui zake. Ni aina gani ya maadui wanaotuweka kifungoni? Na je, tunawezaje kuwa huru?

Mungu ni nani. Tunahitaji kukumbushwa kila mara Mungu ni nani, na kwamba bila yeye hatuwezi lolote. Tutapata picha ya haraka ya tabia ya Mungu. Tutagusia masuala kama vile Utatu Mtakatifu, Baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Tutazungumzia kuhusu Neno la Mungu, na jinsi Yesu alivyozaliwa na bikira Mariamu.

Kuketi, Kuenenda, Kupinga. Kama mwanafunzi wa Yesu Kristo ni muhimu kujua na kufahamu unajifunza nini na kwa njia gani. Labda utaona kwamba kuna mambo mengi tofauti utakayohitaji kujifunza. Mara nyingi mafundisho na masuala ya imani huelekea kuleta mabishano au kupingana yenyewe kwa yenyewe.

Kwa mfano, tukitaka kuishi maisha matakatifu, tunahitaji kufanya bidii. Lakini kwa upande mwingine, neema ipo kila wakati tunaposhindwa. Kwa hiyo tufanye nini sasa? Tutende mema, au tuishi maisha yale ya zamani (yasiyompendeza Mungu) na kuingojea neema ya Mungu?

Wazo la Kuketi, Kuenenda na Kupinga litatoa ufumbuzi wa mgongano huu. Katika kitabu cha Waefeso, masuala yote hayo matatu yamezungumziwa. Tunamshukuru pia sana ndugu Watchman Nee kwa kitabu chake kiitwacho: “Sit, Walk and Stand” (Kuketi, Kuenenda na Kupinga).

Kuketi: Katika Waefeso 2:6 tunasoma maneno yafuatayo ”Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu.” Mungu anataka tujue kwamba Yesu alimaliza kazi yote muhimu pale msalabani kwa ajili ya wokovu wetu. Kazi iliyomalizika ya msalaba na ufufuo wa Yesu, imetufanya kuwa viumbe vipya. Utu wa kale ulitoweka, tukazaliwa mara ya pili. Tunahitaji kujua kwamba Mungu ndiye aliyeifanya kazi hiyo, sisi hatukufanya lolote ila tu kupokea kazi aliyoimaliza. Haijalishi makosa mangapi tunayoweza kufanya, msamaha unapatikana. Hatupo tena chini ya sheria.

Kuenenda: Neno la Mungu katika Waefeso 4:1 linasema, ”Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa.” Kwa kuwa sasa umejua wewe ni nani katika Yesu, unatakiwa kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo. Usiwe sheria bali kiumbe hai ndani ya Roho Mtakatifu. Umeitwa kuenenda na kuishi katika utakatifu na haki. Hii sio njia ya kupata wokovu au upendeleo kwa Mungu bali kuyafanya maisha yako ya nje yalingane na maisha ya kiroho yaliyopo ndani yako. Kila wakati jambo hili liwe chaguo lako. Ndege ni lazima aishi kama ndege, hana chaguo, lakini Mkristo anaweza kuchagua kuishi kama mwenye dhambi. Hii ni hatari, kwa sababu kama Mkristo ataishi kwa muda mrefu katika dhambi bila kuungama na kutubu, ni wazi atarudi nyuma kiroho.

Katika Luka 9:23-24 tunasoma maneno yafuatayo: “Akawambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu ndiye atakayeisalimisha.” Tumeitwa kuyakana au kuyakataa maisha yetu ya zamani na kuukubali msalaba.

Hivi sasa, tumeingia katika agano la damu kati yetu sisi na Mungu; na agano la damu linahitaji vifo viwili. Yesu alishamaliza kazi yake, sisi nasi tumeitwa tufanye sehemu yetu.

Kupinga: Hii ni nia yetu dhidi ya adui. Kuna nguvu kubwa juu ya adui kwa njia ya msalaba. Katika Waefeso 6:10-13 tunaagizwa kuzipinga hila za Shetani. Kutakuwa na vita na shida, lakini Roho Mtakatifu atatupatia faraja. Katika Waefeso 6:11 tunaambiwa “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.” Tunahitaji kujua kwamba Shetani yupo na anatenda kazi; na kwamba matakwa yake ni kuua, kuiba na kukuharibu wewe na familia yako. N kweli yupo! Atakudanganya na kukufanya uamini kwamba huna nafasi ya kuketi. Atakujaribu uenende katika njia za ulimwengu na katika utu wako wa kale. Yesu alimshinda Shetani, hata hivyo anaruhusiwa kutudanganya na kutujaribu. Lakini tunao uwezo wa kumshinda. Maisha haya ya Kikristo sio rahisi. Hisia zetu na mazingira hujaribu kutudanganya kuhusu kuketi, kuenenda na kupinga. Lakini kama tukimpinga Shetani, baada ya kujua sisi ni akina nani katika Kristo, na baada ya kuenenda katika Roho na katika toba, tunaweza kumpinga hadi ushindi unapopatikana.

Mpaka siku tutakapokwenda mbinguni, tutaendelea kuhusika katika vita kubwa dhidi ya ufalme wa Shetani. Ushindi utapatikana kila wakati kama tutazingatia kuketi, kuenenda na kupinga.

“Watu na wakushukuru, Ee Mungu, Watu wote na wakushukuru. Nchi imetoa mazao yake MUNGU, Mungu wetu, ametubariki” (Zaburi 67:5,6)