Mfululizo wa Semina Sehemu ya 1 – Kukua au Kufa Sehemu ya 2 – Damu na Moto

Kitabu cha Mwongozo wa Uanafunzi wa Yesu

Kozi ya mwanzo kwa ajili ya kuishi na kuzaa matunda katika ufalme wa Mungu kwa ushindi na malengo

International School of The Bible (Shule ya Kimataifa ya Biblia) Na Larry Chkoreff

Kukua au Kufa – Mfululizo wa Semina

Na Larry Chkoreff

Jina la Kitabu la asili: Grow or Die Kimetafsiriwa na: Christopher Frank Kimehaririwa na: Rev. Masalu

Kukua au Kufa kimechapishwa na International School of the Bible –ISOB (Shule ya Kimataifa ya Biblia), Marietta, GA USA. Kitabu hiki ni mtaala wa uanafunzi wa Yesu katika shule hii. Barua Pepe: book@isob-bible.org

Kitabu hiki ni mali ya International School of the Bible. Kinaweza kuchapishwa tena, iwapo tu kitachapishwa chote, kwa ajili ya kukisambaza bure (bila malipo). Hairuhusiwi kukibadili au kukihariri kwa njia yoyote ile. Kikichapishwa tena ni lazima kiwe na tangazo la haki miliki (“Copyright © 2001 ISOB”). Kitabu hiki kisiuzwe (au kutumika kutangazia ubora wa bidhaa yoyote iliyokwishauzwa) bila ruhusa ya International School of the Bible (ISOB).

Kwa ajili yako

Kufa

Kukwama kama mfungwa katika Nchi ya Ahadi

Yaliyomo

Ukurasa
UTANGULIZI 6
SEHEMU YA 1 – SEMINA YA 1 11
SURA YA 1 - MATUNDA 12
SURA YA 2 - MTO UTIRIRIKAO 22
Kiambatisho F 38
SURA YA 3 - WAFUNGWA KATIKA NCHI YA AHADI 44
SURA YA 4 - MUNGU NI NANI 52
SURA YA 5 - KUKETI 62
SURA YA 6 - KUENENDA 73
SURA YA 7 - KUPINGA 79
SEHEMU YA 2 – SEMINA YA 2 90
SURA YA 8 – NGUVU YA KUPIGA MBIO KATIKA MASHINDANO – UTANGULIZI 91
SURA YA 9 - NGUVU YA KUPIGA MBIO KATIKA MASHINDANO – MSALABA 94
SURA YA 10 - NGUVU YA KUPIGA MBIO KATIKA MASHINDANO - UKOMBOZI 117
SURA YA 11 - NGUVU YA KUPIGA MBIO KATIKA MASHINDANO – UBATIZO KATIKA ROHO MTAKATIFU 126
KIAMBATISHO A – ORODHA YA MASOMO YA ISOB 137
KIAMBATISHO B – JINSI YA KUENDELEA KATIKA ISOB 141

Mpendwa msomaji:

Baada ya kumfuata Yesu kwa shauku, tangu mwaka 1979, ameniagiza kuandika mambo aliyonitendea siku hadi siku. Ingawa hakuna njia ya mkato ya kuzaa matunda, au ya kukuza uhusiano wako na Yesu, kuna kanuni ambazo nimejifunza zinazoweza kukuondolea miaka mingi ya maumivu na hali ya kukata tamaa katika maisha yako.

Kitabu hiki ni muhtasari wa yale yaliyomo katika kozi inayohusu Kukua au Kufa, ijulikanayo kama “Mfululizo wa Semina”. Kina semina mbili. Semina ya 1 (Sehemu ya 1) ina “masomo saba ya mwongozo.” Semina ya 2 (Sehemu ya 2) ina masomo manne ya ufuatiliaji. Masomo haya 11 yamechukuliwa kutoka katika kozi kamili ya Kukua au Kufa yenye masomo zaidi ya 90.

Kozi yote ya Kukua au Kufa inapatikana kwa mtu binafsi na/au vikundi kwa ajili ya kuwafundisha watu. Baadhi ya masomo hayo yanaendelea kutafsiriwa kwa lugha ya Kifaransa na Kihispania.

Baadhi ya vikundi vimeanzisha shule zinazotoa ushauri (katika nchi kadhaa duniani). Shule hizi huitwa “International School of the Bible” (ISOB), yaani Shule ya Kimataifa ya Biblia. Baadhi ya vikundi hutumia masomo haya wakati vinapokutana ili kujifunza kwa pamoja. Na watu binafsi wamekuwa wakijifunza wenyewe.

Kozi ya Kukua au Kufa kwa sasa inatolewa kama semina kwa Wainjilisti katika nchi kadhaa. Semina hizo huchukua kati ya masaa 4 hadi masaa 14.

Tungefurahi kukusaidia na wewe uanzishe mahali pa kutolea ushauri au mafundisho. Katika hali ya kumuomba Mungu, tutatafakari pia ombi au hitaji la kufanyiwa semina katika eneo lako.

ISOB haidai malipo kwa masomo yake nje ya gharama za kuyatoa au kuyachapisha kwa mara ya pili. Masomo haya hupatikana pia katika diski (CD ROM) kwa ajili ya kompyuta za “Windows” na “Macintosh” kwa bei nafuu.

Tunakubariki katika safari yako na Yesu.

Larry Chkoreff Rais International School of the Bible (Shule ya Kimataifa ya Biblia)

Kitabu hiki ni kwa heshima ya rafiki yangu kupita wote, mke wangu nimpendaye sana, mcha Mungu, Carol, ambaye kwa miaka mingi amenitia moyo kuandika masomo haya, na hatimaye kuyaweka pamoja katika kitabu.

Shukrani maalum zimwendee ndugu Jim Crawford wa “Project Light” ambaye amekuwa rafiki wa thamani sana na mfariji katika kazi hii.

Ninaomba sala hii kwa kila mtu atakayesoma kitabu hiki.

Msalaba Asante Bwana kwa ushindi wa msalaba wa Yesu Kristo.
Asante kwa kuwa tulisulibiwa na wewe
Kuzimu Asante Bwana kwa kuvumilia mateso na kifo na kushuka
hadi kuzimu kwa ajili yetu.
Ufufuo Asante Bwana kwamba ulifufuliwa kutoka katika wafu, na
kwamba sisi nasi tulifufuliwa pamoja na wewe na kuketi
pamoja na wewe katika ulimwengu wa roho, ndani yako Kristo.
Ujazo Asante Yesu kwa kutujaza Roho Mtakatifu
Mateso Asante Yesu kwa kuona kwamba tunastahili kushiriki mateso
yako.
Ushindi Asante Bwana kwa ushindi uliotuahidia katika maisha haya
na yale ya milele.

Utangulizi

Je umewahi kujisikia huna malengo au matumaini? Umewahi kujisikia kana kwamba uko juu ya gurudumu kama fuko ndani ya kizimba lakini huendi popote? Umewahi kujiuliza ni kwa vipi Mungu anatazamia uishi maisha ya ushindi. Unaweza kujisikia kwamba Mungu atakupeleka mbinguni siku fulani, lakini unaona kana kwamba Mungu amekuacha bila msaada. Sawa, kama umekuwa katika hali hiyo, fahamu kwamba hata watu wanaomwamini Yesu Kristo hujisikia hivyo mara kwa mara.

Wakati mwingine inaonekana kwamba lengo letu ni kujaribu kupata ushindi au mafanikio katika maisha kwa nguvu zetu wenyewe. Kwa mama mzazi, lengo lake linakuwa ni kuwafundisha watoto wake wamche Mungu, kuwalisha na kuwatunza. Kwa mke, lengo linakuwa ni kutafuta kuwa karibu na mume wake na kuwa salama na kuwa na mawasiliano mazuri. Kwa mume, lengo lake mara nyingi ni kujaribu kuilisha familia na kujaribu kuonekana mtu wa maana, anataka wengine wamstahi. Kwa kijana, lengo lake linaweza kuwa ni kutafuta kujua nafasi aliyo nayo katika jamiii ni ipi, kutafuta kazi na mwenzi wa maisha. Na mara nyingi lengo letu ni kujaribu kutatua matatizo mbalimbali katika maisha. Hata hivyo, mambo haya yakifanikiwa mara nyingi huwa tunajisikia watupu bila kuwa na lengo jingine zaidi, au yasipofanikiwa huwa tunajisikia kukata tamaa na kukosa matumaini.

Jibu ni nini? Kama Neno la Mungu linavyosema katika Wagalatia 2:20, tukisulibiwa pamoja na Kristo, na Kristo akiwa hai ndani yetu, basi hatutajisikia vizuri mpaka pale tutakapolifanya lengo la Mungu kuwa lengo letu.

Naamini kwamba Mungu ana malengo mengi kwa ajili yetu katika maisha. Hata hivyo, malengo yake yote yako chini ya lengo moja kubwa na la msingi: KUMLETA BIBI ARUSI KWA YESU.

Kitabu cha Waefeso kinatupa ufahamu. Katika Waefeso 4:11-13 Paulo anaonyesha kwamba lengo au makusudi kamili ya huduma ni kuujenga mwili wa Kristo ili ufikie "cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo." Katika Waefeso 4:12b tunajifunza kwamba tunatakiwa kuujenga Mwili wa Kristo. Na katika Waefeso 5:25-27 tunaona kwamba pamoja na kumleta bibi arusi kwa Kristo, Yesu anataka bibi arusi wake asafishwe ili atakapopelekwa kwake awe mtakatifu asiye na mawaa.

Mwili au Kanisa ni bibi arusi wa Kristo. Neno la Mungu katika Waefeso 5:32 linazungumzia juu ya siri ya Kristo na kanisa kwamba inafanana na mume na mke. Mstari huo unasema hivi: "Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa."

Arusi ya Mwanakondoo na bibi arusi inaonekana kuwa ni mojawapo ya matukio ya mwisho karibu na mwisho wa Kitabu cha Ufunuo wa Yohana. Katika Ufunuo wa Yohana 19:7 tunasoma maneno yafuatayo: "Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari."

Hii haimaanishi kwamba sisi sote tunahitaji kwenda nchi za nje na kuhubiri katika mitaa kama mwinjilisti. Hapana, kila mtu amepewa karama na Mungu kwa njia ya kipekee. Kazi (ya kumleta bibi arusi kwake) aliyotupatia tunaweza kuifanya. Kila mtu ana umuhimu wake. Fikiria jambo hilo. Kama kuna mtu mmoja tu anayepaswa kuwa bibi arusi miongoni mwa Kanisa lakini bado hajafanya hivyo, basi bibi arusi hajakamilika. Kwa kuwa bibi arusi anahitaji kuendelea kukua mpaka awe mtu mzima, basi kazi yetu haijakamilika. Mungu anaweza kukuita uombe, au umpende jirani yako, au uende nchi ya mbali. Ni Mungu tu anayejua mambo aliyo nayo kwa ajili yako.

Tunapaswa kujiona kama chembe ya mchanga ufukweni. Ni kama vile hatuonekani, hata hivyo, bila sisi, ufukwe haujakamilika. Mungu anatuhitaji tufanye sehemu yetu.

Agano la Kale linatupa picha ya moyo wa Mungu jinsi anavyojisikia kuhusu jambo hili.

Hawa alitoka katika ubavu wa Adamu. Kanisa lilitoka katika ubavu wa Kristo pale msalabani.

Angalia Mwanzo 24. Ibrahimu (mfano wa Baba) anamtuma mtumishi wake (mfano wa Roho Mtakatifu – aliye ndani yako na ndani yangu) kutafuta mke kwa ajili ya mtoto wake Isaka (mfano wa Yesu).

Maneno ya Mungu katika Mwanzo 24:4-9 yanasema, “bali enenda hata nchi yangu, na kwa jamaa zangu, ukamtwalie mwanangu Isaka mke. Yule mtumishi akamwambia, Labda yule mwanamke hatakubali kufuatana nami mpaka nchi hii, je! Nimrudishe mwanao mpaka nchi ulikotoka? Ibrahimu akamwambia, Ujihadhari, usimrudishe mwanangu huko. BWANA, Mungu wa mbingu, aliyenitoa katika nyumba ya babangu, na kusema nami katika nchi niliyozaliwa, aliniapia akisema, Nitawapa uzao wako nchi hii; yeye atampeleka malaika wake mbele yako, nawe utamtwalia mwanangu mke tokea huko; na yule mwanamke asipokubali kufuatana nawe, basi, utafunguliwa kiapo changu hiki; lakini usimrudishe mwanangu huko. Yule mtumishi akaweka mkono wake chini ya paja la Ibrahimu bwana wake, akamwapia katika neno hilo.”

Soma habari yote hiyo katika Mwanzo 24. Yule mtumishi akampata Rebeka, aliyekuwa akiwanywesha maji ngamia, na kisha akampa maji ya kunywa alipofika katika eneo lile. Hii ilitokea “kabla hajamaliza kuzungumza” (sura ya 24: 15). Na kabla hajatamka yale maneno, Rebeka alijitokeza akatimiza yale maneno.

Katika Mwanzo 24:64-67 tunasoma maneno yafuatayo: “Rebeka akainua macho, naye alipomwona Isaka, alishuka juu ya ngamia. Akamwambia mtumishi, Ni nani mtu huyu ajaye kondeni kutulaki? Mtumishi akasema, Huyu ndiye bwana wangu. Basi akatwaa shela yake akajifunika. Yule mtumishi akamwambia Isaka mambo yote aliyoyatenda. Isaka akamwingiza Rebeka katika hema ya mama yake, Sara, akamtwaa Rebeka, akawa mkewe, akampenda; Isaka akafarijika kwa ajili ya kufa kwa mamake.”

Hiyo ni njia nzuri ya kupata picha ya moyo wa Mungu! Baba alikusudia kupata mke kwa ajili ya mtoto wake, lakini siyo mke tu bali yule

“Ibrahimu akamwambia mtumishi wake, mzee wa nyumba yake, aliyetawala vitu vyake vyote, Tafadhali uutie mkono wako chini ya paja langu.” (Mwanzo 24:2).

Angalia, Ibrahimu hakumtuma mtumishi yeyote tu. Alimtuma yule aliyetawala vitu vyake vyote. Katika kitabu cha Mathayo 24 tunapata habari ya mtumwa aliyewekwa juu ya vitu vyote. Hebu tuone mambo tunayoweza kujifunza kwake. Habari yenyewe ipo katika Mathayo 24:42-51.

Kwanza, mtumwa yule alijiweka tayari kwa ujio wa Bwana wake. Hii inamaanisha kwamba tunapaswa kujiweka tayari kumlaki Yesu atakapokuja tena duniani, lakini pia tunapaswa kuwa tayari kumlaki Yesu sasa anapokuja kuangalia jinsi tulivyo waaminifu kuyatunza yale tuliyopewa.

Mtumwa alikuwa mwaminifu. Kuwa mwaminifu katika madogo ni jambo muhimu kwa Mungu. Mungu anapenda kujua jinsi tunatenda mambo yetu ya kila siku katika maisha yetu. Mungu hawezi kutupatia zaidi mpaka kwanza tuwe waaminifu kwa madogo aliyotupatia. Tunahitaji kuwa waaminifu katika mambo ya kimwili na mambo ya kiroho.

Mtumwa alikuwa pia mtoaji. Aliwapa watu wengine chakula. Katika Mathayo 24:46 imeandikwa hivi: “Heri mtumwa yule, ambaye bwana wake ajapo atamkuta akifanya hivyo.”

Mtumwa hakuwatenda vibaya wengine. Mtumwa hakuishi kama watu wasioamini. Mtumwa alikuwa na hekima. Ni wazi kwamba hekima hii siyo ya

dunia, ni hekima ya Mungu.

Katika 1 Wakorintho 2:6-8 tunaambiwa hivi: “Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika; bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu; ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu.”

Katika 1 Wakorintho 1:23-24 tunaambiwa kwamba Kristo aliyesulibiwa, ni hekima.

Naamini, kwamba hekima ya kweli kutoka kwa Mungu imehifadhiwa kwa ajili ya wale waliopita katika mauti. Imehifadhiwa kwa ajili ya wale waliopoteza matumaini, maono, ndugu zao, kazi, heshima na kadhalika. Kitabu cha Ayubu sura ya 28 kinazungumzia kutafuta hekima. Kwamba hekima haionekani katika nchi ya walio hai. Hii inamaanisha kwamba mauti tu ndiyo imeiona. Yule tajiri katika Mathayo 19 alikuwa na mengi ya kutumainia katika dunia.

Unapojua kwa hakika kwamba “mfumo wa dunia” na juhudi zako mwenyewe hazitoi matumaini, basi wewe unaweza kupata hekima. Ukiangukia katika kundi hili, nyanyua kichwa chako kwa matumaini, kwa kuwa Mungu atakutendea mambo ya kupita kawaida!

Maisha yanaweza kuwa magumu, lakini tunaweza kuishi kwa ushindi tukimwangalia Yesu siku zote.

Watu, wahudumu, marafiki, au hata makanisa yanaweza kutukatisha tamaa, lakini Yesu hawezi kufanya hivyo kamwe. Katika Waebrania 2:8b-9 tunaambiwa kwamba hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake, ila twamwona Yesu aliyeionja mauti kwa ajili yetu. Tunapotambua yale aliyoyafanya Yesu kwa ajili yetu na kujua Yeye ni nani, tunampenda.

Tunapompenda, tunaridhika kujua kwamba tunaishi kwa ajili ya makusudi yake na kwamba jambo hilo linampendeza.

Jambo zuri ni kwamba tunapopita katika hatua hii, tunamwangalia Yesu wakati wote, tunatenda kazi kwa ajili yake, tunapita katika majaribu kwa ajili yake na kumtumikia. Wakati macho yetu yanapomwangalia, Yeye anakuwa thawabu yetu. Hatuhitaji kuangalia jinsi ya kubadili tabia, au jinsi ya kutimiza mahitaji yetu, au hata huduma. Tunatakiwa tu kumwangalia Yeye na kuunganishwa naye. Tunaiona “neema ya ajabu” ya Mungu ikitufunika. Napenda kukuambia kutokana na uzoefu wangu kwamba jambo hili huweza kumfanya mtu astahimili nyakati ngumu katika maisha na kuwa na furaha.

  1. Tunda la Roho. Mtumishi huyu alikuwa na tabia ya Mungu.
  2. Tunda la kutimiziwa mahitaji yake yote. Katika Mwanzo 24:10 utaona kwamba Baba alimpa yule mtumishi yote aliyoyahitaji kwa ajili ya safari, siyo tu ngamia 10, bali mambo yote aliyoyahitaji.
  3. Tunda la huduma. Mtumishi huyu alishiriki kumpendeza baba na Mwana kwa kumleta nyumbani bibi arusi.

Hayo ndiyo mambo yanayohusu uanafunzi wa Yesu na ndiyo yaliyozungumziwa katika kitabu hiki.

Kuzaa matunda katika maisha yetu kwa ajili ya ufalme wa Mungu katika maeneo yote hayo matatu. Ubarikiwe.

Sehemu ya 1 – Semina ya 1

Sura ya 1-7 zinazungumzia:

  1. Tunda
  2. Mto Utiririkao
  3. Wafungwa katika Nchi ya Ahadi
  4. Mungu ni nani
  5. Kuketi
  6. Kuenenda
  7. Kupinga